Home | News & Events | Contact Us
 
 
 
 
 
 
 
 

News Subscription

 Your name:
 

 Email Address:
 

SALAMU ZA MKURUGENZI MKUU KWA WAFANYAKAZI WOTE WA MAMLAKA YA VIWANJA VYA NDEGE KWA KUMALIZA MWAKA 2004 NA KUANZA MWAKA MPYA WA 2005.


Ndugu Wakurugenzi, Wakuu wa Vitengo, Mameneja, Wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi na Wafanyakazi wote - Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania.

Kwa niaba ya Uongozi wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania na kwa niaba yangu binafsi, nachukua fursa hii fupi kuwapeni pongezi kwa kumaliza mwaka wa 2004 na kuanza mwaka mpya wa 2005.

Ni matumaini yangu kuwa kila mmoja wetu anayo furaha isiyopimika kwa kubarikiwa  nafasi hii ya pekee.

Hivyo basi sote hatuna budi kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa rehema zake alizotujalia na kutufikisha hapa tulipo.

Katika kuifurahia  nafasi hii ni vema kukumbuka na kutafakari kwa makini ili kuona ni mambo yapi tulitarajia kuyafanya kwa kipindi cha mwaka tunaoumaliza na kwa kiwango gani  tumetekeleza au tumefikia katika utekelezaji wake, au kukwama na kuchambua changamoto zilizotukabili katika utendaji wa kazi zetu.

Kwa kufanya hivyo tunajiweka katika nafasi ya kujua wapi tulipofika, na misingi iliyotufikisha hapo.

Tukiwa tumejua mahali tulipo, ni wajibu wetu kutazama mbele ili kuona ni mahali gani tunatarajia kufika katika kipindi kinachofuata na kutambua mambo ambayo tunapaswa kuyafanya, hasa tukitilia maanani  kukidhi mahitaji ya wanaotumia huduma zetu na hivyo kufikia malengo tuliyojiwekea.

Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania kama mdau katika sekta ya usafiri wa anga ina malengo na majukumu ambayo ni changamoto kubwa kwa Mamlaka yenyewe, Taifa na Ulimwengu kwa ujumla.

Changamoto hizi zinatokana na mfumo mzima wa mabadiliko yanayotokea ulimwenguni hususan katika sayansi na teknolojia. Sekta ya usafiri wa anga ni moja ya maeneo ambayo yameendelea na mabadiliko makubwa na ya haraka ambayo yanahitaji kufuatiliwa kwa karibu ili kuweza kuhimili ushindani katika utoaji huduma kwa misingi ya biashara.

Katika salamu zangu nilizotoa mwaka jana, nilieleza baadhi ya mambo ambayo Mamlaka yetu ilikuwa inakabiliana nayo kama changamoto; hii ikiwa ni pamoja na :

*           Uhaba/upungufu wa fedha kutokana na uchache wa vyanzo vya mapato ikilinganishwa na mahitaji makubwa ya ukarabati, ujenzi na uboreshaji wa miundo mbinu ya viwanja vya ndege.

*           Hali isiyoridhisha ya Viwanja vyetu vya Ndege hususan uchakavu na upungufu           wa  vifaa na miundo mbinu.

*           Kuendelea kwa vitendo vya ugaidi kuwa tishio kwa maangamizi ya mali na maisha ya watu  katika sekta nzima ya usafiri wa anga.

*           Janga la Ukimwi ambalo linaendelea kuwa tishio la “nguvu kazi” katika utendaji wa shughuli za Mamlaka na Taifa kwa ujumla.

Napenda nitamke wazi kuwa mambo haya bado ni changamoto kubwa hadi leo na bado juhudi za pamoja zinahitajika ili kuendelea kukabiliana nayo katika kipindi kinachofuata.

Hata hivyo, kwa niaba ya Uongozi wa Mamlaka , nawajibika kutoa shukrani za dhati kuwa katika kipindi cha mwaka 2004, tumekuwa na maelewano ya Kiwango cha juu kati ya viongozi na watumishi katika sehemu mbalimbali za kazi katika kukabili changamoto hizo.

Wafanyakazi wote kwa pamoja na kila mmoja kwa nafasi yake mmeonesha uwezo na ushirikiano mkubwa wa kiutendaji. Hali hii imebainisha kujengeka na kukua kwa umoja na kutambua umuhimu wa mshikamano miongoni mwetu katika utendaji wa majukumu tuliyokabidhiwa. Napenda niwashukuru sana kwa hili na kuwaomba tuongeze juhudi za kudumisha umoja wetu.

Katika mwaka tunaomaliza wa 2004, tulitarajia kufanya yafuatayo ikiwa ni sehemu tu ya mambo mengi :-


(i)    Kukamilisha taratibu za uhamisho wa moja kwa moja wa wafanyakazi.  Matarajio

       yalikuwa suala hili likamilike ndani ya miezi mitatu (3) ya kwanza ya mwaka 2004.          

·        Nashukuru kwamba suala hili lilikamilika na hivyo kuondoa hofu iliyokuwa imewagusa watumishi kuhusu hatima ya utumishi wao.

(ii) Kuimarisha ushirikishwaji wa Wafanyakazi katika maamuzi na mipango ya Mamlaka kupitia Baraza la Wafanyakazi.

·        Kufuatia kuundwa kwake mwezi Novemba 2003, baraza la Wafanyakazi limekuwa chombo muhimu kinachosaidia Uongozi wa Mamlaka katika kufanya maamuzi ya kiuendeshaji. Katika kipindi cha mwaka 2004, Baraza lilifanya vikao viwili kwa mujibu wa Mkataba.

(iii)  Kuendelea kukamilisha taratibu za ajira kujaza nafasi zilizokuwa wazi kwa kuzingatia  mahitaji ya kazi, kadiri itakavyojitokeza.

·        Taratibu za ajira ziliendelea kufanyika kwa kuzingatia umuhimu ili kujaza nafasi zilizo kuwa wazi na hivyo kupunguza uzito wa kazi kwa watumishi wengine.

(iv)  Kukamilisha taratibu za upimaji wa wazi wa utendaji kazi (OPEN PERFORMANCE                                         REVIEW AND APPRAISAL SYSTEM – OPRAS) kuanzia Julai 1, 2004.

·        Kutokana na sababu zisizozuilika, lengo hili halikufikiwa kama ilivyokuwa imekusudiwa. Hata hivyo, nashukuru kwamba kwa kiasi kikubwa baadhi yenu pamoja na kutopewa mafunzo, wamefanya juhudi za kutengeneza mikataba ya utendaji (Performance Agreement) na kuisaini. Natumaini kuwa mikataba hiyo itaendelea kuwa miongozo katika utendaji kazi za kila siku na hatimaye kutumika katika upimaji wa utendaji kazi.

(v) Kuimarisha na kuboresha utendaji wa kazi kwa kutoa mafunzo yanayolenga kuongeza                                            uwezo wa mtumishi kufanya kazi zake kwa umakini na ufanisi zaidi.

·        Juhudi za kutoa mafunzo kwa watumishi ziliendelea, hii ikiwa ni pamoja na kutayarisha Mpango wa Mafunzo (Training Program). Hata hivyo kutokana na hali isiyoridhisha ya uwezo wa kifedha wa Mamlaka, utoaji wa mafunzo ulielekezwa kuwawezesha watumishi kuongeza uwezo wa kufanya kazi kwa umakini na ufanisi zaidi.

(vi) Kuendelea na ujenzi wa kiwanja cha Ndege cha Songwe - Mbeya.

·        Ujenzi wa Kiwanja cha ndege cha Songwe uliendelea kwa kasi ya kuridhisha.

(vii) Kuendelea na ukarabati wa mfumo wa umeme kwenye kiwanja cha ndege cha        Kimataifa cha Dar es Salaam ambao ulitarajiwa kukamilika ifikapo mwishoni mwa mwaka 2004.

·        Kazi ya ukarabati wa mfumo wa umeme iliendelea vizuri na ilikamilika mwezi Mei 2004 (kabla ya muda uliokuwa umetarajiwa).

(viii) Kuendelea na juhudi za kuimarisha hali ya usalama (safety and Security) kwenye        viwanja vya ndege kulingana na viwango vya ICAO.

·               Pamoja na kutoa mafunzo yanayohusika, utekelezaji wa "Airport Security Programme na Airport Emergency Plan" kila kiwanja, Mamlaka iliendelea na juhudi za kutoa vifaa vinavyohusika na kujenga uzio kwa kuzingatia uwezo wa kifedha wa Mamlaka na kutoa kipaumbele kwa maeneo hayo mawili yaani "safety & security".  Kitengo kipya cha “Compliance” kimeanzishwa kulingana na muundo wa Mamlaka, kwa ajili ya uthibiti wa ndani ili kujihakikishia  kuwa tunakidhi viwango vya ICAO vya “Safety & Security” kabla ya ukaguzi.

(ix)              Kuendelea na juhudi za kutafuta vyanzo vipya vya mapato na kuboresha vile vilivyopo           ili   kuendelea kujenga uwezo wa Mamlaka kifedha.

 

·        Mamlaka iliendelea na juhudi za kutafuta vyanzo vipya vya mapato na kuboresha vile vilivyopo ili kuendelea kujenga uwezo wa Mamlaka kifedha; hii ikiwa ni pamoja na kuweka misingi ya kushirikisha sekta binafsi katika uwekezaji kwenye viwanja vyetu vya ndege.

(x)   Kuendelea kushirikiana na wadau katika kuanzisha maeneo huru ya utengenezaji na   usafirishaji bidhaa nje ya nchi (Export Processing Zone) kwenye Viwanja vya Ndege hususan DIA.

·        Kutokana na sababu zisizozuilika, Mamlaka haikuweza kufanikiwa sana katika suala hili. Bado juhudi zinaendelea kulifanyia kazi zaidi.

(xi)  Kukamilisha marekebisho ya Muundo wa Mamlaka na hatimaye kufanya tathmini ya                              kazi (Job Evaluation and Regrading) pamoja na kurekebisha muundo wa Mishahara.

·        Marekebisho ya muundo wa Mamlaka yalikamilika na kuidhinishwa ndani ya kipindi cha nusu ya kwanza ya mwaka 2004. Utakelezaji wa muundo huo ulianza mwezi Julai 2004. Ni matumaini yangu kuwa muundo huu mpya utasaidia kuboresha utendaji kazi na uwajibikaji ndani ya Mamlaka.

·        kufuatia kurekebishwa muundo, zoezi la tathmini ya kazi limeanza na linatarajiwa kukamilika ndani ya miezi mitatu ya kwanza ya mwaka 2005.

·        Hata hivyo, wakati tathmini ya kazi inaendelea uongozi wa Mamlaka uliofanya hatua ya muda mfupi kwa kuongeza mishahara ya watumishi kwa viwango vya kati ya asilimia 26 (26%) kwa kima cha juu na asilimia 42 (42%) kwa kima cha chini.

(xii)    Kuendele ana juhudi za kuunganisha mitandao ya mawasiliano katika shughuli zetu na   kati ya viwanja, na kupevuka katika matumizi ya teknolojia ili ituwezeshe kuboresha na kurahisisha utoaji wetu wa huduma na pia kuongeza mapato.

·        Kazi hii bado imeendelea kufanyika

(xiii)    Kukamilisha mkakati wa upatikanaji wa fedha za mradi wa ukarabati wa viwanja kadhaa              (11) vilivyowekewa kipaumbele maalumu.

·        Bado juhudi zinaendelea kufanyika kwa kuwasiliana na taasisi na vyombo mbalimbali ili kutafuta fedha za kutuwezesha kukarabati viwanja vilivyowekewa kipaumbele maalum.  Fedha za kukarabati “runway” na Apron za DIA Terminal II zilipatikana na mradi unaanza Januari 2005.

Ndugu Wafanyakazi wenzangu, utekelezaji wa malengo haya ulikwenda vizuri kwa kiasi kikubwa katika baadhi ya maeneo na vile vile maeneo mengine utekelezaji wake haukwenda vizuri kama niliyoelezea. Aidha katika salaam zangu za kila mwaka nimekuwa nikizungumzia mafanikio tuliyoyapata na changamoto tulizokabiliana nazo. Tulitafakari na kupima utendeji wetu wa kila mwaka kipekee. Ilibidi iwe hivyo kwani “”KILA SAFARI HUANZA KWA HATUA MOJA BAADA YA NYINGINE”

Ndugu wafanyakazi, kuzungumzia mafanikio na mupungufu yaliyojitokeza kiutendaji ndani ya mwaka mmoja hadi mwingine na nini tufanye kukabiliana na changamoto hizo kumetujengea misingi ambayo inaweza kuwa vigumu kuiwekea viwango vilivyofikiwa kwani si kila kitu hupimwa na kupata uhalisi wake. Mafanikio yanaweza kuonekana katika uhalisi au vinginevyo (Quantitative and Qualitative terms)

Leo tunaumaliza mwaka huu wa 2004 huku Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania ikiwa imetimiza miaka mitano (5) tangu ilipozinduliwa rasmi tarehe 03 Desemba 1999. Basi ni vizuri kuweka mawazo yetu ndani ya miaka mitano iliyopita ili tuone tumekua kiasi gani tukiwa tumefika nusu ya safari yetu kuelekea kwenye DIRA tuliyojiwekea wakati Mamlaka inaanzishwa (TAA VISION: TO BECOME A MODEL IN THE PROVISION OF AIRPORT FACILITIES AND SERVICES IN EASTERN AFRICA BY 2010). 

Tukitazama na kutafakari kwa ujumla wa kipindi cha miaka mitano iliyopita, ni dhahiri sote na hata wadau watakubaliana nami kuwa utendaji kazi wa kazi zetu umeendelea kuwa bora. Kwa mfano ndani ya kipindi hicho:

1.      Wadau wetu wemeendelea kutupongeza kwa uboreshaji huduma zetu,

2.      pamoja na changamoto zilizotukabili, tumeendelea kuendesha na kuhakikisha viwanja vyetu viko katika hali ya kuruhusu ndege, abiria na mizigo kupata huduma wanazostahili,

3.      tumekuwa tukipewa pongezi na tuzo kwa ushiriki na mchango wetu kwenye shughuli mbali mbali za kijamii na kitaifa kama vile Janga la moto kwenye kituo cha mafuta cha TANESCO - Ubungo, Wiki ya Taifa ya Usafirishaji na wiki ya usalama wa usafiri wa anga na kadhalika.

4.      tarehe 17/12/2004, Taasisi iitwayo “FOUNDATION FOR EXCELLENCE IN BUSINESS PRACTISE (FEBP)” ya Uswisi iliitunukia Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania Medali ya Dhahabu (Gold Medal Award) kutokana na juhudi za Mamlaka za kuendeleza uboreshaji wa huduma zake kwa msingi ya kibiashara.

Baada ya tafakari ya mwaka 2004 na kwa ufupi kabisa miaka mitano iliyopita ikiwa ni nusu ya safari kufikia kwenye lengo kuu, naomba nitoe mwelekeo au matarajio ya kipindi cha miaka mitano inayofuata kama ifuatavyo:

1.   Tumetumia miaka mitano iliyopita kuweka mipango mingi ya utekelezaji na kuweka muundao unaofaa kutuwezesha kufikia malengo yetu.  Pamoja na kuendelea na kupanga ni matarajio yangu kuwa tutatumia muda mwingi zaidi katika miaka mitano ifuatayo kwa utendaji wa  yale tuliyokwisha kupanga, hususan mipango itakayoboresha mapato na huduma kwa kushirikisha sekta binafsi.

2.    Mwelekeo muhimu pia ni ule wa kila mtumishi kutenda kazi anayotarajiwa kutenda; kila mmoja kwa nafasi yake; na kwa ukamilifu na muda uliopangwa.  Ni kwa jinsi hiyo tu tunaweza kuionea fahari Mamlaka yetu na kisha kujivunia mafanikio yatakayotokana na utendaji wetu bora, na pia kustahili kuzungumzia kuitendea haki Mamlaka  kwa kuifanyia kazi iliyokuweka ndani yake.

3.            Kuendeleza juhudi za kukabiliana na changamoto zilizopo na zitakazojitokeza ili kuboresha huduma zetu kwa wateja kwa kuhakikisha kuwa viwanja vyetu ni salama katika utoaji wa huduma bora kadiri inavyostahili.

4.            kuendelea na ujenzi wa kiwanja cha ndege cha Songwe hadi kukamilika kwake kwa muda  uliopangwa.

5.            Kuendeleza juhudi za uimarishaji wa mapato ya Mamlaka ili kuijengea uwezo wa kifedha.

6.            kuendeleza juhudi za uboreshaji na upanuzi wa huduma za viwanja vya ndege kwa kushirikisha sekta binafsi kadiri inavyowezekana.

7.            kuendeleza juhudi za uboreshaji wa mazingira ya kazi na kujenga raslimali watu (Human Resources) yenye uwezo wa  kutoa huduma bora kwa ufanisi zaidi.

8.            kuendeleza juhudi za kupambana na janga la UKIMWI ambalo ni tishio kwa raslimali watu ndani ya Mamlaka na Taifa kwa ujumla.

Malengo haya yaangaliwe katika mtazamo wa muda mrefu (miaka mitano ijayo) na katika kipindi cha muda muda mfupi kila idara, kiwanja au sehemu ya kazi inapaswa kuyaainisha na kuweka mikakati ya utekelezaji. Aidha mikakati hii ya utekelezaji ijumuishwe katika mipango ya kazi (work plans) itakayoandaliwa.

Ndugu wafanyakazi, matarajio haya ni baadhi tu ya mengine mengi ambayo si rahisi kuorodhesha yote, na yanahitaji ushirikiano, juhudi na maarifa ya kila mmoja wetu. Kwa kuzingatia hali ya ushirikiano, michango ya mawazo na juhudi na maarifa ambayo tumekuwa nayo kwa kipindi cha miaka mitano (5) iliyopita tangu kuanzishwa kwa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania, naamini kuwa malengo yetu yatafikiwa.

Pamoja na juhudi na ushirikiano tulionao katika utendaji wa kazi zetu ndani ya Mamlaka ya Viwanja vya Ndege, sisi ni sehemu ya jamii katika Taifa letu la Tanzania. Kwa kiasi kikubwa tunawajibika kuungana na juhudi za kitaifa katika mapambano dhidi ya janga la UKIMWI, umaskini na uharibifu wa mazingira.

Napenda nichukue nafasi hii kuwaomba viongozi na watumishi wenzangu wote kwenye sehemu mbalimbali za kazi kuendelea kuzungumzia na kuhimiza mapambano dhidi ya UKIMWI, umaskini na uharibifu wa mazingira kama majukumu yetu ya kazi.

Mwisho, narudia tena kuwashukuru kwa ushirikiano wenu mliouonyesha kwangu katika utendaji wa kazi katika kipindi cha mwaka 2004 na kwa kipindi chote cha miaka mitano iliyopita hadi kufikia hapa tulipo. Natumaini kuwa ushirikiano huu utaimarishwa na kudumishwa zaidi katika mwaka wa 2005.

Nawapa hongera kwa kumaliza mwaka 2004 na kuwatakia heri na baraka katika mwaka 2005.

Ahsanteni.

 

Eng. P. F. H. Tesha
 MKURUGENZI MKUU

Advertisements

 
Terms and Conditions - Copyright: Tanzania Airports Authority - 2003
Suggestions & Comments to: Webmaster. - Last Updated: 10/04/2003